Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

Familia ya Lissu Yatoa Msimamo Wake Matibabu ya Lissu

Familia ya Lissu Yatoa Msimamo Wake Matibabu ya Lissu

Familia ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu imesema ataendelea kupata matibabu kwenye Hospitali ya Nairobi, Kenya wakati taratibu za kumhamisha zikiendelea.

Aidha, familia hiyo imesema itaweka wazi kwa umma siku itakapomhamishia hospitali nyingine mtaalamu huyo wa sheria.

Akizungumza na Nipashe kwa simu jana, kaka wa Lissu, Vicent Lissu, alisema mbunge huyo atahamishwa kutoka katika hospitali hiyo kwenda kupata matibabu ya kibingwa zaidi kama ilivyoelezwa Jumanne iliyopita na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.

"Mheshimiwa Lissu bado anaendelea na matibabu kwenye hospitali ileile," Vicent alisema, "akihamishwa mtajua maana tutaeleza ila kwa sasa bado ni mapema kusema atakwenda nchi gani, itoshe kujua bado yupo Nairobi."

Alipoulizwa kuhusu gharama za matibabu ya mbunge huyo na kama kuna deni lolote katika Hospitali ya Nairobi, Vicent alisema:
"Hilo ni suala binafsi sana na sidhani kama ni wakati wake kulizungumzia, jueni anaendelea na matibabu.

"Mengine ni masuala ya kifamilia sana."

Hadi jana jioni, dola za Marekani 31,663 (Sh. milioni 69.9) zilikuwa zimechangwa na watu walio ughaibuni kugharamia matibabu ya Lissu, ikiwa ni ongezeko la dola 1,969 (Sh. milioni 4.36) kutoka zilizokuwa zimechangwa wakati Mbowe akizungumza na waandishi wa habari kwa mara ya mwisho jijini Dar es Salaam kuhusu hali ya Lissu.

Kwa mujibu wa mtandao wa www.gofundme.com/Lissumedicalcare, tangu utaratibu huo wa watu walio ughaibuni kumchangia Lissu uanzishwe Septemba 12 na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, mtu aliyetoa mchango mkubwa zaidi ni Yasinta Massawe aliyechangia dola 3,000 (Sh. milioni 6.6).

Mbowe aliwaambia waandishi wa habari Jumanne kuwa michango hiyo imetokana na uhamasishaji unaofanywa na Watanzania walio nje wakiongozwa na Mange Kimambi anayeishi Marekani.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Mbowe alisema afya ya Lissu imeimarika na ameshaanza kula na kupumua bila msaada wa mashine.

Siku moja baada ya mkutano huo, picha za mnato na video zilianza kusambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii zikimwonyesha Lissu akifanyishwa mazoezi akiwa kwenye kiti cha wagonjwa na nyingine mbunge huyo akisikika akimshukuru Mungu na watu wote waliopambana kuhakikisha wanaokoa maisha yake.

Katika mkutano wake wa Jumanne, Mbowe alisema Lissu ambaye amefanyiwa operesheni 17 hadi Oktoba 12, gharama za matibabu yake zilikuwa zimefikia Sh. milioni 412.45.

"Tumepokea michango mingi ambayo imewezesha kwa kiwango kikubwa kusaidia matibabu ya Mheshimiwa Lissu," Mbowe alisema. "Kundi la kwanza katika kuchangia ni wabunge wa Chadema ambao walichanga Sh. milioni 48.4.

"Wananchi na viongozi wengine wa chama walichanga Sh. milioni 24.2, wanachama na viongozi na familia walichanga kupitia akaunti maalum ya CRDB Sh. milioni 90.8, michango iliyochangwa na wabunge wote Sh. milioni 43.

"Wapo Watanzania kwenye anga ya kimataifa walichangia fedha dola za Marekani 29,700 ambapo dada zetu kina Mange Kimambi walisaidia kuhamasisha kupitia mitandao.

"Hata mpaka sasa hivi bado fedha hazijatosha.

"Hapa ninazungumza gharama ya matibabu pekee yake kwa mwezi Septemba zimegharimu fedha za Kenya Sh. 10,687,316 sawa na dola za Marekani 106,875 na ilipofika Oktoba 12 jumla ya gharama ni Sh. 13,708,156 za Kenya."

Mbowe pia alisema jopo la madaktari 12 ambao walikuwa wanamtibu Lissu wamelipwa Dola za Marekani 46,440 (Sh. milioni 102.5) kwa kuwa kila daktari anapotoa huduma kwa muda fulani anahitajika kulipwa.

Lissu (49), ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS) alihamishwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwenda Nairobi usiku wa Septemba 7 baada ya kupigwa risasi 32 na watu wasiojulikana, akiwa ndani ya gari lake nyumbani kwake Area D mjini humo. 

Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017