Na Saleh Ally
UKIJUMLISHA mabao yaliyofungwa na timu za Ruvu Shooting, Stand United, Njombe Mji, Ndanda FC na Lipuli ya Iringa ndiyo unapata idadi ya mabao 21 yaliyofungwa na Simba katika mechi 9 za Ligi Kuu Bara.
Achana na kwamba bado mashabiki wa Simba wanaendelea kulalamika kwamba timu yao haifungi mabao, lakini imefikisha mabao 21 katika mechi 9 tu. Huku timu inayoifuatia Simba ni Yanga yenye mabao 11, tofauti ya mabao 10.
Timu ya tatu kwa kufunga mabao ni Prisons ya Mbeya yenye 10, maana yake kama utawajumlisha walio katika nafasi ya pili na tatu kwa ufungaji mabao ndiyo utapata idadi ya mabao waliyofunga Simba.
Pia unaweza kutumia lugha laini, kwamba Simba imeizunguka Yanga mara mbili na chenji katika ufungaji wa mabao. Wakati huo, nikiwa ninakukumbusha kwamba Yanga ndiyo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara.
Hakuna ubishi kwamba Yanga sasa wanapambana kuhakikisha wanautetea ubingwa wao kwa mara nyingine na tunaweza kukubali kwamba hawako mbali sana kwa kuwa wako katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 17 wakati vinara Simba wana 19.
Kikubwa ambacho unaweza kukumbuka ni kwamba msimu uliopita, bingwa na aliyeshika nafasi ya pili walifungana kwa pointi na mwisho mabao ya kufunga na kufungwa yaani goal difference-GD, ikaamua bingwa na akawa Yanga.
Maana yake, Kocha George Lwandamina kama anashindana na Simba au Azam FC wanashindana pia basi ni lazima wabadilishe mwenendo.
Kwamba wanavyokwenda, Simba inaonekana kujiwekea akiba kubwa ya mabao ya kufunga huku wakiendelea kuwa na ngombe ngumu pia kwa kuwa wameruhusu mabao manne huku Yanga wakiwa wamefungwa matano.
Katika hali ya kawaida unaweza kuangalia hali ilivyo na utaona Kocha George Lwandamina wa Yanga, anajitutumua kwelikweli lakini hauwezi kumlaumu kutokana na hali ilivyo. Najua umewahi kusikia nje ya uwezo, hii inamkuta yeye.
Washambulizi ambao ndiyo wamesajiliwa kwa ajili ya kufunga mabao, Donald Ngoma na Amissi Tambwe, wote wamekuwa majeruhi kwa kipindi kirefu sasa.
Tambwe anaonekana kuwa majeruhi kwa muda mrefu kwa kuwa tangu msimu uanze hajawahi kuingia uwanjani kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara. Maana yake, amekosa mechi tisa.
Kama atarejea, bado hatakuwa na nafasi ya kufanya vizuri haraka. Atataka muda kujenga tena hali ya kujiamini na kurejea katika moto wake ambao ulimfanya kuwa mfungaji bora mara mbili na mara moja akashika nafasi ya pili.
Maana yake, haitakuwa ndani ya mechi tatu zijazo au ikiwa hivyo itakuwa imetoa bahati nzuri jambo ambalo halipaswi kulitegemea.
Ukimzungumzia Ngoma raia wa Zimbabwe, ingawa wengi wanaona kama yeye ana nafuu kwa kuwa angalau amecheza ligi ya msimu huu na kufunga. Lakini usisahau Yanga ilimkosa kwa kipindi kirefu mwishoni mwa msimu uliopita hadi kukawa na tuhuma kwamba alikuwa akiifanyia Yanga “mchezo” ingawa zilikanushwa.
Kama Lwandamina ataendelea kuwasubiri Ngoma na Tambwe, ninaamini ataendelea kuwa katika wakati mgumu na huenda akapoteza uhakika wa mambo mawili. Kwanza pointi na pili mabao mengi, jambo ambalo anapaswa kulipa kipaumbele.
Kama Lwandamina ataendelea kuwasubiri Tambwe na Ngoma, ligi haitamsubiri yeye. Hivyo huu wakati kuelekea katika dirisha dogo la usajili, anapaswa kufanya uamuzi mgumu kuhakikisha anabadili mambo.
Kusema anamuacha Ngoma au Tambwe na kuongeza mshambulizi mmoja ambaye ni bora na anaweza kumsaidia kupata mabao yatakayozalisha pointi ni jambo analotakiwa kulifanya sasa.
Kuumia si jambo la makusudi, aliyeumia anapaswa kupewa moyo kwa kuonyeshwa kwamba anathaminiwa. Lakini ukweli haufichiki kwamba; Yanga inataka ushindi, inataka mabao mengi na inataka kuwa bingwa tena. Hivyo walio wagonjwa, hawawezi kuisaidia!
Lwandamina anaweza akawa na nafasi ya kuchagua mwenyewe. Awaridhishe Ngoma na Tambwe au Wanayanga wote kulingana na wakati. Huenda anaweza kupima kwa kuona wakati sahihi wachezaji wake hao wanaweza kuwa wamerejea.
Kama bado itakuwa kuna ugumu na inaonekana matibabu yanahitaji angalau mwezi mwingine mmoja. Basi bila shaka aamue kumuacha mmoja wao na kumsajili mtu mwingine atakayemsaidia kutimiza malengo.
Kumbuka Yanga wanaingia katika michuano ya kimataifa na wanahitaji mtu sahihi kulingana na ugumu wa ligi ya Mabingwa Afrika. La sivyo wataangukia pua mapema.
Tena unapaswa kukumbuka, sasa tegemeo ni Ibrahim Ajibu na Obrey Chirwa, hii inaonyesha Yanga haijakaa vizuri kwa maana ya kikosi imara kwa kuwa kama ataumia mmoja wapo. Pilau litakuwa “limechacha” hata kabla ya sherehe.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini