Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

Rais Magufuli Atoa Maagizo Mazito Kwa Waziri wa Ujenzi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutafuta fedha na kujenga barabara ya Mutukula – Minziro yenye urefu wa kilometa 6 ili kurahisisha usafiri wa watu na mizigo.

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo tarehe 11 Novemba, 2017 katika Mji wa Mutukula mpakani mwa Tanzania na Uganda baada ya kupokea kero za wananchi waliokusanyika jirani na geti la kuvuka mpaka huo ambao wamedai kukosekana kwa barabara hiyo kunawalazimu kutumia barabara ya kuzunguka Kyaka.

Pamoja na kumtaka Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kujenga barabara hiyo Mhe. Rais Magufuli pia amewataka viongozi wa Mkoa wa Kagera kufanyia kazi madai ya wananchi waliolalamikia kupata usumbufu katika kizuizi cha Kyaka jirani na mto Kagera.

Hata hivyo Mhe. Dkt. Magufuli amewataka wananchi wa Mutukula kutambua kazi ya ulinzi na usalama inayofanywa na vyombo vya dola na amewataka kutoa ushirikiano kwa viongozi na Serikali katika kuhakikisha mpaka huo unakuwa salama.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi hao kuongeza juhudi katika shughuli za maendeleo zikiwemo kilimo na biashara na amerejea agizo lake la kuutaka Mkoa wa Kagera kujenga soko la kimataifa katika maeneo ya jirani na mpaka huo ili wananchi wapate mahali pa kuuzia bidhaa zao kwa njia halali.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mutukula
11 Novemba, 2017

Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017