Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

USAJILI : Yanga Kuleta Mkali Zaidi Ya Ajibu


MABOSI wa Yanga chini ya Kocha Mkuu, Mzambia George Lwandamina, wamekiangalia kikosi cha Simba kilichopo kileleni mwa Ligi Kuu Bara, kisha kuamua kufanya jambo kama litawini ni wazi watani zao hao lazima waombe po!

Kwanza wamempuuza beki wao wa kati wa zamani, Vincent Bossou, aliyewadengulia katika dirisha la usajili lililopita, kisha kutoa baraka zote kwa Mkongomani Fiston Kayembe kuvaa jezi zao, lakini wakaenda mbali zaidi kwa kuamua kumleta straika mkali kuliko Ibrahim Ajibu ili kuimaliza Simba.

Mabosi hao kwa kutambua kuwa dirisha dogo la usajili linafunguliwa wiki ijayo, walikutana faragha na benchi la ufundi na kupeana michongo ya kuweza kuibana Simba kabla ligi haijachanganya na hasa baada ya kuona wamezidiwa ujanja.

Yanga iliyolazimishwa sare mbili mfululizo katika mechi zilizopita ikiwamo ya watani zao Simba waliofungana nao bao 1-1 kabla ya Singida United kuibana na kutoka nao suluhu, imeachwa pointi mbili na Simba katika msimamo wa ligi.

Simba inaongoza ikiwa na alama 19 sawa na Azam, lakini wakiwa na faida ya uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa, wakati Yanga yenyewe ina pointi 17 kama za Mtibwa Sugar, ila uwiano wa mabao unawabeba mbele yao.

Kocha Lwandamina ameuambia uongozi kuwa katika dirisha dogo anataka mastraika wawili tu wa kuimaliza Simba, huku akimfungia vioo Bossou kwa madai hana nafasi tena kwani Kayembe anamtosha kabisa.

Bossou alikataa kusaini mkataba mpya mwanzoni mwa msimu huu akitaka pesa ndefu na kuondoka kwake mpaka sasa kumeifanya eneo hilo la beki wa kati kukosa mbadala, lakini Lwandamina amesema Kayenge atabeba mzigo huo.

MKALI WA AJIBU

Akizungumza na nasi  Lwandamina alisema amewaambia viongozi wa Yanga katika ripoti yake ya awali aliyoiwasilisha mara baada ya kurudi safari yake kuwa anataka kutafutiwa mastraika wawili wenye uwezo wa juu zaidi ya Obrey Chirwa na Ajibu ambao waliofunga mabao manane msimu huu.

Lwandamina alisema anataka kutafutiwa mastraika hao ili kumaliza kazi, lakini akipendekeza mmoja kati yao awe wa kigeni atakayekuwa na sifa kubwa za kupambana zaidi ya wawili hao.

“Tunahitaji kufanya maboresho makubwa kidogo katika safu ya ushambuliaji, ndiyo maana nimewaambia viongozi tunahitaji umakini zaidi kama tulivyofanya dirisha lililopita,” alisema Lwandamina.

“Nataka kuona tunatafuta kwa umakini washambuliaji wawili wa kati. Kwa sasa tunao Ajibu na Chirwa, lakini hao wanaokuja sitaki wawe kama hawa, nataka wawe wakali zaidi na wanaojua kupambana.

“Tukiwapata hao tutakuwa tumefanya kitu kikubwa, lakini hakutakuwa na maana kama tutaleta wenye ubora kama wa hawa tulionao. Nafurahi kuwa na uongozi ambao unaheshimu mapendekezo ya kocha.

“Sio lazima tuwasajili wote tunaweza kumsajili mmoja itategemea na wakati huo ukifika kipi tutakuwa tumekiamua kwa pamoja kati ya wachezaji tulionao na pia tutaangalia wale tuliowapata na uwezo wao.”

NGOMA AU TAMBWE
Endapo Yanga itawapata washambuliaji hao wawili, ni wazi italazimika kuachana na mastraika Amissi Tambwe na Donald Ngoma ama kumbakiza mmoja tu.

Ngoma na Tambwe wako nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya goti na wote ni wachezaji walioibeba timu hiyo katika mafanikio ya misimu miwili iliyopita Yanga ikitwaa ubingwa wa Bara.

Kukosekana kwa nyota hao kumeifanya Yanga kutaabika katika kasi ya ufungaji, japo Ngoma alicheza mechi za mwanzoni na kufunga mabao mawili huku Ajibu na Chirwa wakijitahidi kuibeba wakitupia mabao manane kati ya 11 ya timu yao mpaka sasa katika ligi ya msimu huu.
source:Mwanaspoti

Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017